MAUZO YA MAZAO YA UVUVI YAONGEZEKA, YAFIKIA TRILIONI 2.28

Mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 42,302.03 na samaki hai tani 181,268 mwaka 2021 hadi kufikia tani 59,746.41 na samaki hai tani 148,041 mwaka 2024, huku thamani ya mauzo hayo ikipanda kutoka dola za marekani milioni 457.8 hadi kufikia shilingi trilioni 2.28 kwa mwaka huu.

akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma Jana mei 6, 2025 wakati akieleza mafanikio ya waziri ya mifugo na uvuvi katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, waziri wa wizara hiyo, Dk. Ashatu kijaji amesema juhudi za serikali katika kuimarisha mazingira ya biashara, kupunguza baadhi ya tozo na kufungua masoko ya kimataifa zimesaidia kuongeza thamani na kiasi cha mazao yanayouzwa nje ya nchi.

Dkt. kijaji amesema mafanikio hayo yametokana na mikakati madhubuti ya serikali ya awamu ya sita, ikiwemo kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, kutoa elimu kwa wavuvi na wafanyabiashara, pamoja na kusimamia kwa karibu kanuni na taratibu za biashara ya samaki na mazao yake.

Amesema nchi za Poland, Denmark, Ujerumani, Marekani na uswisi zimeendelea kuwa masoko makubwa ya samaki hai wa mapambo kutoka Tanzania. “Mafanikio haya ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya uvuvi na kuhakikisha watanzania wananufaika na rasilimali za maji tulizonazo.” amesema dk. kijaji.

Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuwavutia wawekezaji na kuongeza tija katika sekta ya uvuvi, hususani katika kuongeza ajira, kipato cha wananchi na mapato ya Taifa.

Post a comment